Na Mwandiahi wa A24tv .
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa niaba ya Kamishna Jenerali *ARETAS JAMES LYIMO* leo tarehe 29.01.2025 imeteketeza Kilogramu 204.8165 za dawa za kulevya katika Dampo la Muriet lililopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika Kilogramu 204.8165 zilizoteketezwa, mirungi ilikuwa ni Kilogramu 172.8165 na bangi kavu ilikuwa Kilogramu 32.0 yote ikihusisha jumla ya watuhumiwa 33 waliokamatwa kwa makosa ya kupatikana na dawa hizo ambapo kati yao watuhumiwa Wanaume walikuwa 25 na Wanawake walikuwa Nane ambapo wote walikamatwa katika operesheni zilizofanyika kuanzia Januari 2024 hadi Januari 27, 2025 katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Taratibu za uteketezaji wa vielelezo hivyo umefanyika kwa kuzingatia sheria na miongozo husika ambapo Mahakama ya Wilaya ya Arusha iliridhia vielelezo hivyo viteketezwe kwa kuwa vikikaa muda mrefu vinaweza kupoteza uhalisia na hata kupelekea kuharibika.
Aidha, Watuhumiwa Saba katika miongoni mwa Watuhumiwa 33 waliokamatwa na dawa hizo zilizoteketezwa hivi punde tayari kesi zao zilishatolewa hukumu za vifungo Mwaka 2024 na kesi nyingine zinaendelea katika Mahakama za ngazi ya Mikoa na Wilaya katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
*_Taasisi za Serikali zilizopo mkoani Arusha zikihusisha Afisa Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Arusha, Afisa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini, Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Arusha na Afisa Mazingira kutoka H/Shauri ya Jiji la Arusha wote hao kwa mujibu wa takwa la kisheria walishiriki katika uteketezaji wa Kilogramu 204.8165 za dawa za kulevya katika Dampo la Muriet jijini Arusha._*
*MWISHO*