Na Geofrey Stephen Arusha.
MRADI wa Tanzania ya Kidijitali unaofadhiliwa na Benki ya Dunia(WB) umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake huku lengo likiwa ni kuweka mazingira wezeshi, kutoa huduma bora na miundombinu wezeshi kwa wananchi ili wanufaike.
Aidha mradi huo ambao unasimamiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma umefanikisha kupeleka wataalamu 50 kusoma shahada ya pili na wengine 400 kupata mafunzo.
Akizungumza jana Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mafunzo na Huduma za Tehama kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ,Mohammed Mshaka,wakati wa kufunga kikao cha kufanya tathimini ya hatua zilizofikiwa alisema mradi huo ulianza mwaka 2021 utakamilika Oktoba 2026.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwezesha wananchi kupata huduma wakati wowote na mahali popote ili kufikia malengo ya uchumi wa kidijitali hususan wananchi wa vijijini na makundi maalum
“Mradi huu mpaka sasa umefanikisha kuunganisha mifumo ya Taasisi 901 kusomana, minara 758 imeondolewa kutoka 2G kwenda 3G pamoja na kuhuisha vifaa ambavyo vimeshasimikwa,kuongeza uwezo wa Intaneti katika Taasisi za serijali ambapo Tanzania Bara inatumia GB 40 na Zanzibar GB 20.
Alisema pia mradi huu umefanikisha kutengeneza vituo 30 vya kuwezesha wananchi kupata huduma muhimu sehemu moja, pamoja na kutengeneza mifumo ya kutoa huduma ambayo ni jamii namba, jamii ‘X-change’ na mfumo wa huduma za malipo (Cashless)
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mkataba,Kazi Serikalini Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Tairo alisema mradi huo umesaidia serikali kutumia mfumo wa kielekroniki wa upimaji utendaji kazi kwa watumishi wa umma (PERMIS &PIPMIS na tathimini ya mahitaji ya rasilimali watu.
Wakati huo huo, Kiongozi wa Timu ya wataalamu wa mradi huo kutoka Benki ya Dunia (WB) Paul Seaden alisema, mradi huo unaendeshwa kipindi cha miaka mitano ambapo unashughulikia maeneo Anuwai, zinazounga mkono nguzo tofauti za mkakati wa uchumi wa dijiti, ikiwemo kuwainua wananchi kiuchumi maeneo ya vijijini.
Alisema lengo kuu ni kuwafikia watanzania kupata huduma za uhakika katika kiwango kinachotakiwa cha utoaji wa huduma za dijiti kwa serikali, ikiwemo uanzishwaji wa vituo vya duka moja nchini kote pamoja na kuanzisha mtandao wa vituo vya utoaji wa ujuzi wa dijiti na uandishi wa dijiti .
Aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika uchumi wa kidigiti, ambayo yamefanywa hadi sasa na kufikia asilimia 80, ya utoaji huduma kimifumo pamoja na jamii kwa ujumla, lakini pia mradi huo umehusisha makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu.
Mwisho