.Watu Saba wakiwemo wanakwaya Sita wamefariki dunia papo hapo huku wengine 23 wakijeruhiwa baada ya gari walikokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo na kupinduka katika milima ya Pare, Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo, ambapo amesema ajali hiyo imetokea leo asubuhi majira ya saa nne, Machi 30, 2025 eneo la barabara ya Bangalala wakati wanakwaya hao wakitokea Chome kuelekea Vudee wilayani humo.
“Leo majira ya saa nne katika barabara ya Bangalala, Wilaya ya Same, kumetokea ajali ya gari aina ya coaster lililokuwa limebeba wanakwaya ambao walikuwa wanatokea Chome kuelekea Vudee, ambapo wanakwaya 6 wamefariki duniani na kusababisha majeruhi 23,”amasema DC Mgeni
Aidha amesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya gari walikokuwa wakisafiria kufeli break na kupoteza mwelekeo na kupelekea kupinduka katika milima hiyo.
“Hawa wanakwaya walikuwa wamepanda gari aina ya coaster sasa walipofika barabara ya Bangalala gari lilifeli break na kuanza kurudi nyuma nyuma na ndipo liliposerereka na kupinduka na kusababisha vifo vya wanakwaya Sita na majeruhi 23,”amesema DC Mgeni
DC Mgeni amesema miili ya wanakwaya hao, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya ya Same.
Akitoa salamu za pole kwa familia hizo, DC Mgeni amesema wanaendelea kuziombea familia ambazo zimepoteza wapendwa wao na kuwaombea subira katika kipindi hiki cha majonzi.
“Mungu aziweke mahali pema peponi roho za marehemu amina,”
Mwisho.