Na Mwandishi wa A24tv.
Arusha.
Wanawake wa kikundi cha ‘Arusha Super Woman’ wamefanikiwa kutembelea wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha sambamba na kutoa msaada wa vitu mbalimbali vya usafi, lishe, na kujisitiri.
Mbali na vifaa hivyo pia wamelipia baadhi ya wagonjwa bili zao walizokuwa wanadaiwa yenye thamani ya shilingi milioni 1.4.
Wakikabidhi msaada wa vitu hivyo, Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Arusha Super Women,’ Bertha Kondo, amesema kuwa wameamua kutoa msaada huu kwa wazazi na wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kama sehemu ya kutekeleza mpango wao wa kugusa maisha ya jamii.
“Tumekuwa tukitoa misaada katika kambi mbalimbali na kwa wafungwa gerezani, lakini awamu hii tumekuja hapa Mount Meru ili kuwatembelea wagonjwa, kuwafariji katika kipindi kigumu cha ugonjwa wanachopitia”
“Faraja hii tumeambatanisha na kutoa msaada wa vitu mbalimbali vya usafi, lishe, na kujisitiri, ili kuwaonyesha kuwa tuko pamoja na uponyaji pia upo” amesema Bertha.
Mlezi wa kikundi hicho, Stephania Boniface, amesema wametoa vitu mbalimbali kama sabuni za kipande, sabuni za unga, dawa za mswaki, maziwa ya watoto njiti, pampasi, na taulo za wanawake.
“Vilevile, tuliguswa na baadhi ya wagonjwa waliolazwa hapa ambao walikuwa wameshindwa kulipa bili zao za matibabu” amesema na kuongeza
“Hivyo, tumewalipia bili za matibabu yenye thamani ya jumla shilingi milioni 1.4 ili kuwasaidia kuondokana na deni hilo,” amesema Stephania.
Amesema kuwa msaada huo zaidi wametoa kwenye wodi za wanawake wajawazito, waliojifungua na wodi ya watoto njiti kwa kutambua umuhimu wa malezi kwa mtoto.
“Bado dunia tunaadhimisha mwezi wa siku ya mwanamke, ndio maana tumetoa kipaumbele kwa wanawake wenzetu ambao wameamua kulea na wengine wamevuka kiunzi za mimba na sasa wamejifungua”
Mmoja wa wagonjwa walipokea msaada huo Stellah John amesema kuwa amesema kuwa wamefarijika kuna jinsi wanawake wenzao wamejitoa kuwapa faraja
“Kiukweli inatia moyo na kufariji sana na inaleta hamasa hata kwa sisi tuliko hapa kwamba tukitoka salama tuje kukumbuka kurudi kuona wenzetu, watakaokuwa hapa” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wengine kujitokeza kutoa misaada katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika hospitali kwani wako wengi ambao wanaugua na hawana msaada wala ndugu wa kuwahudumia wala kuwalipia bili.
Mwisho….