NA: Maipac Team- Eyasi
maipacarusha@gmail.com
Wanawake wa Jamii ya wahadzabe wanaoishi katika eneo la Eyasi wilayani Karatu Mkoani Arusha wamepaza sauti katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa kumuomba Rais Samia Suluhu asikilize kilio chao.
Wakizungumza katika mdalaho wa siku ya wanawake, uliofanyika katika Kijiji cha Qandet eneo la Eyasi wilaya ya Karatu, kwa kuandaliwa na taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) kwa kushirikiana na Kituo cha Radio cha SAVVY FM, Wanawake hao, wameeleza wanakabiliwa na changamoto lukuki.
Katibu wa Wahadzabe eneo la Eyasi, Maria Yona anasema wanamuomba Rais Samia kuwasaidia wapate ardhi, maji, chakula na kuzuia uvamizi wa ardhi yao.
“Tunatamani sana kumuona Rais Samia Mwanamke mwenzetu, tumweleze sisi wanawake wa Kihadzabe tunaishi katika maisha magumu sana, hatuna maji, hatuna ardhi na chakula”anasema
Anasema ardhi yao ya asili inaendelea kuvamiwa na wakulima na kusababisha kukosa hadi chakula cha asili, ikiwepo matunda, mizizi na asali.
Maria anasema, wanawake wa jamii ya Kihadzabe ni masikini sana na hawajawahi kufikiwa hata na mikopo midogo midogo ya halmashauri kama walivyo wanawake wengine.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahadzabe, Mdindi Samboga anasema wanawake na wanajamii wengine wa kihadzabe, wanaiomba serikali kuwamilikisha ardhi yao kama ilivyo jamii nyingine.
“Wahadzabe wenzetu wa yaeda chini, wilaya ya Mbulu wamepata hati miliki ya kimila za maeneo yao hivyo hawavamiwi sana na sisi tunaomba kusaidiwa” anasema
Mhadzabe mwingine, Ng’o Nkoo anasema hawajuwi maana ya maadhimisho ya siku ya wanawake, kwani wao hawajawahi kushiriki lakini kubwa maisha yao yamekuwa ya shida sana.
“hatuna ardhi, hatuna chakula, vijana wanashindwa kuoa kwa sababu hakuna Wanyama na asali ya kupeleka mahari na Chanzo cha haya ni ardhi yetu ya asili kuendelea kuvamiwa”anasema
Afisa Maendeleo ya jamii kata ya Baray, Kassim Miraji anakiri kuwa wanawake wa jamii ya kihadzabe bado hawajafikiwa na mikopo na kutokana na maombi yao, watafanyia kazi suala hilo.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu imetoa fedha za mikopo kwa wanawake na katika eneo hili mimi ndio napaswa kushughulikia ninaahadi kuanzia leo ntaanza kuwasaidia kujiunga katika vikundi ili wanufaike na mikopo”anasema
Mwenyekiti wa bodi ya Utalii katika eneo la Lake Eyasi, Daniel Hhawu anasema ni kweli jamii ya Kihadzabe wakiwepo wanawake wanakabiliwa na shida nyingi licha ya kuwa kivutio cha watalii.
“Ni kweli ardhi yao inavamiwa na wanakosa chakula ila mambo haya yapo chini ya serikali sisi kama bodi ya Utalii katika eneo hili hatuhusiki na masuala ya ardhi na kilio chetu tunaomba wasaidiwe”anasema
Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma anasema wameamua kuifikia jamii ya Wahadzabe ili kujua changamoto za jamii hiyo hasa wanawake na Watoto.
“Wameeleza shida ya ardhi yao kuvamiwa, wameeleza kukosa maji, chakula cha asili na huduma nyingine muhimu lakini pia tumehamasisha wajitokeze kushiriki katika uchaguzi mkuu, kwa kugombea nafasi mbali mbali”anasema
Kaimu Meneja wa SAVVY FM, Neema Twazihirwa akizungumza katika mdahalo huo, anasema radio yao kwa kushirikiana na MAIPAC wataendelea kushirikiana na jamii ya Wahadzabe kupaza sauti zao juu ya kero zinazowakabili.
Twazihirwa anasema wao kama wanahabari, wataaandaa vipindi maalum ambavyo vitasaidia kupaza sauti za jamii hiyo, ili waweze kupata misaada mbali mbali.
Katika Maadhimisho hayo, MAIPAC na SAVVY FM pia walitoa msaada wa vitu mbali mbali kwa wanawake wa jamii ya Kihadzabe na Watoto.
Katika kuelekea maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wanawake Duniani, MAIPAC na SAVVY FM kwa msaada wa wadau mbali mbali ikiwepo wafanyakazi wa UN Women imewasafirisha wanawake wa jamii hiyo, kuhudhuria sherehe za kitaifa jijini Arusha, Machi 8, katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
MWISHO.