Na Mwandishi wa A24tv.Arusha
Licha ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Divisheni ya Biashara, kuamuru kufutwa kwa hisa asilimia 18 zilizokabidhiwa kwa Daudi Ibrahim Lumala kinyume na utaratibu, pamoja na kufutwa kwa nafasi yake kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Sunset Tarangire Limited, Lumala bado ameendelea kuwepo ndani ya kampuni hiyo.
Picha ni Daudi Ibrahim Lumala aliyekua Mkurugenzi Mwenza .wa kampuni ya Sunset Tarangire limited
Aidha, kikao cha wanahisa kinatarajiwa kufanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kabla ya kumalizika kwa siku 30 zilizopangwa, kutokana na kuwa Mfanyabiashara maarufu nchini, Saleh Salim Alamry, ambaye mahakama ilimhakikishia ushindi katika shauri hilo, yupo mahabusu katika Gereza la Kisongo akisubiri kesi nyingine inayomkabili ambayo mashitaka yake hayaruhusu dhamana.
Pia, ofisi za kampuni hiyo zimefungwa baada ya kushindwa kulipa kodi, hali iliyotokea wakati Daudi Lumala akiwa anaendesha kampuni hiyo, ingawa haijafahamika ni kiasi gani cha kodi kinachodaiwa wala muda ambao kodi hiyo haikulipwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha juzi, Wakili wa Alamry, Okare Joshua Emesu, alisema baada ya kuona upande wa pili unakaidi amri ya mahakama, waliamua kuwasilisha uamuzi huo kwenye mamlaka mbalimbali za serikali na taasisi za kifedha ili utekelezwe.
“Tumefanikisha kufunga akaunti zote za benki za kampuni ya Sunset Tarangire, na taratibu zinaendelea kupitia Msajili wa Makampuni (BRELA) ili kumtoa Lumala kwenye hisa za kampuni na ukurugenzi kama mahakama ilivyoelekeza,” alisema Emesu na kuongeza:
“Kwenye kikao cha wakurugenzi, ajenda kuu itakuwa juu ya kughushi hisa na uteuzi wa kiholela wa Mkurugenzi Daudi Ibrahim Lumala na mustakabali wa uendeshaji wa kampuni utajulikana hapo.”
Hata hivyo, Okare alisema kuwa tayari amewasilisha polisi malalamiko ya mteja wake Alamry dhidi ya wanahisa wenzake raia wa Saudi Arabia, Abdulkarim na Khaled Alrajhi, akiwatuhumu kwa kughushi hisa na kufanya uteuzi wa mkurugenzi kiholela.
Malalamiko hayo yamesajiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kwa RB namba ARS/RB/7321/2024 ambapo polisi wameeleza kuwa uchunguzi unaendelea.
Awali, Aprili 4, 2025, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ilitoa uamuzi uliomtangaza mfanyabiashara maarufu Saleh Salim Alamry kama mtu aliyekuwa anatendewa isivyo halali na kampuni ya Sunset Tarangire Limited.
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Abdallah Gozi katika Shauri Namba 20496/2024, ambapo mahakama ilisikiliza hoja na ushahidi wa pande zote mbili kabla ya kutoa uamuzi.
Katika uamuzi huo, mahakama iliagiza mabadiliko yote yaliyofanyika ndani ya mfumo wa BRELA kuanzia mwezi Mei 2024 yafutwe, ikiwemo uteuzi wa Daudi Ibrahim Lumala kama Mkurugenzi na Mwanahisa wa kampuni hiyo. Mahakama ilitamka kuwa uteuzi huo ulikuwa batili na haukufuata taratibu za kisheria.
Pia, mahakama iliagiza kufutwa kwa hisa asilimia 18 zilizokabidhiwa kwa Daudi Lumala kinyume cha utaratibu, pamoja na kufutwa kwa nafasi yake kama Katibu wa Kampuni.
Katika agizo jingine, mahakama imeamuru kuitishwa kwa kikao cha wanahisa na wakurugenzi halali ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya hukumu kwa ajili ya kujadili hatma ya kampuni hiyo.
Katika shauri hilo, Alamry, aliyeko mahabusu katika Gereza la Kisongo kwa kesi nyingine, aliwakilishwa na Wakili Faisal Rukaka, huku upande wa kampuni ukiwakilishwa na Wakili Mnyiwala Mapembe waliomtetea Khaled Mohamed Alrajhi, Abdulkarim Mohamed Alrajhi, Daudi Ibrahim Lumala na kampuni ya Sunset Tarangire Limited.
Maombi yaliyowasilishwa na Alamry yalikuwa manane, ambapo Mahakama ilikubali sita kati ya hayo, huku ikitupilia mbali maombi yote kumi yaliyowasilishwa na upande wa wajibu maombi.
Katika maombi hayo, upande wa Alamry uliomba Mahakama itamke kuwa hatua zilizochukuliwa na kampuni hiyo hazikuwa za haki, mchakato wa kumpatia Daudi Lumala hisa na madaraka ulikuwa batili, na kwamba kikao halali cha wanahisa kitangazwe — maombi yote haya yakakubaliwa.
Kwa upande wa wajibu maombi, waliomba pamoja na mengine Mahakama itamke kuwa Alamry hana haki ndani ya kampuni na mali zote ziwe chini ya kampuni, lakini maombi hayo yote yalitupiliwa mbali.
Shauri hili limevuta hisia za wengi kutokana na ukubwa wa kampuni na jina la mfanyabiashara anayehusishwa, huku hatua za utekelezaji wa maamuzi ya mahakama zikisubiriwa ndani ya siku 30.