Na Geofrey Stephen Handeni .
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewaagiza wakuu wa shule na walimu kuhakikisha wanaweka mkazo katika kuimarisha maadili na ufaulu wa wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari wilayani humo.
Akizungumza leo wakati wa ziara ya kukagua shule za msingi Mlimani, Vibaoni na Chanika, Mhe. Nyamwese alisema kuwa ni jukumu la viongozi wa shule kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora itakayomwezesha kufaulu na kuwa raia mwema katika jamii.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya alikagua miundombinu ya shule, ikiwemo hali ya madarasa, vifaa vya kujifunzia, mazingira ya walimu na wanafunzi pamoja na kuzungumza moja kwa moja na walimu na wanafunzi kwa lengo la kusikiliza changamoto na kutoa hamasa ya kitaaluma.
“Tunahitaji kuona matokeo mazuri. Kila mmoja wetu anapaswa kuwajibika katika nafasi yake kuhakikisha Handeni inakuwa kinara katika ufaulu wa kitaifa. Elimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa,” alisisitiza Mhe. Nyamwese.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Mkuu wa Wilaya kutembelea shule mbalimbali kwa ajili ya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sera na mikakati ya elimu. Aliongozana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Bi. Magreth Killo, Afisa Tarafa wa Chanika Bi. Julieth Mushi, watendaji wa mitaa la maafisa kutoka Halmashauri va Mii Handeni.