Na Mwandishi wa A24tv Handeni Tanga .
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI
anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, ameongoza kikao kazi kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya afya katika Halmashauri zote mbiliza Wilaya hiyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, Wakurugenzi wa Halmashauri ya Mii Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Aidha,watendaji wa sekta ya afya kutoka serikalini katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Halmashauri walishiriki kwa pamoja kuwasilisha taarifa, kutoa maoni na kujadili changamoto za utekelezaji wa huduma za afya katika maeneo yao.
Katika kikao hicho, Prof. Nagu alipokea taarifa za maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya afya, hali ya upatikanaji wa rasilimali watu, hali ya vifaa tiba, na utekelezaji wa shughuli za afya za msingi. Alieleza kuwa lengo la Serikali kupitia TAMISEMI ni kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati, na kwa ubora unaokubalika.
Mhe. Nyamwese alieleza kuwa Wilaya ya Handeni inatekeleza kwa bidii maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya, na akaeleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa, wataalamu, na wadau umechangia mafanikio yaliyopo.
Prof. Nagu alipongeza Wilaya ya Handeni kwa juhudi hizo na akaahidi kuwa Serikali itaendelea kupeleka rasilimali na kushughulikia changamoto zilizowasilishwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.
Mwisho .