Na Geofrey Stephen Arusha .
Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, ameielekeza Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Utumishi wa Umma (TAPA-HR) kuanza mchakato wa kuanzisha bodi ya taaluma kwa kada hiyo. Lengo kuu ni kudhibiti ukiukwaji wa maadili, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza tija kazini.
Akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa TAPA-HR unaofanyika kwa siku nne jijini Arusha, Mhandisi Zena alisema bodi hiyo itakuwa chombo muhimu katika kusimamia taaluma ya watumishi wa kada ya rasilimali watu na utawala, na kuondoa sintofahamu zilizopo kuhusu utekelezaji wa maadili ya kazi
Mkutano huo unaongozwa na kaulimbiu: “Mwelekeo Mpya wa Nafasi ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala: Kusukuma Mabadiliko, Kuendana na Mageuzi na Teknolojia kwa Ajili ya Kuboresha Huduma katika Utumishi wa Umma.”
Mhandisi Zena alibainisha kuwa bodi hiyo itakuwa kiunganishi muhimu kati ya wataalamu hao na Chuo cha Utumishi wa Umma kwa madhumuni ya kuhuisha maudhui ya kitaaluma na kuhakikisha viwango vinavyohitajika vinafikiwa. Pia alizitaka taasisi zinazohusika kuandaa miongozo mipya itakayosaidia kuboresha utendaji kazi na weledi.
“Muundo wa sasa wa utumishi umezidiwa na wakati. Kuna umuhimu wa kuhuisha ili uendane na mahitaji ya sasa, kasi ya teknolojia na matarajio ya Watanzania,” alisisitiza. Aliongeza kuwa bodi hiyo itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaasisi, kutoa mwongozo wa nidhamu kazini, na kusuluhisha malalamiko kuhusu ukiukwaji wa kanuni.
Alihimiza matumizi ya mifumo ya kidijitali iliyoandaliwa na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, akisema itasaidia kupunguza mianya ya rushwa na kuongeza uwazi katika utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Mrope, alisema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/2050 utakuwa mwongozo muhimu kwa wataalamu hao kukabiliana na changamoto za kiteknolojia na kisera zinazojitokeza.
Mwenyekiti wa TAPA-HR, Bi. Grace Francis, alisema chama hicho kimejikita katika kukuza taaluma za wanachama wake, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni muundo wa kazi usioendana na hali halisi ya sasa. Aliiomba serikali kushughulikia suala hilo kwa dharura.
Naye Katibu Tawala Msaidizi wa Menejimenti ya Ufuatiliaji na Ukaguzi wa Serikali za Mitaa mkoa wa Arusha, Bw. Ramadhani Madeleka, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa huo, alisema serikali ya mkoa wa Arusha inafurahia kuandaa mkutano huo na kuhakikisha usalama umeimarika kwa washiriki.
Mkutano huo umehusisha zaidi ya washiriki 999 kutoka kada mbalimbali, huku tukio hilo pia likishuhudia uzinduzi wa tovuti rasmi ya Jumuiya pamoja na utoaji wa tuzo kwa watumishi bora wa kada hiyo.
Mwisho