Na Geofrey Stephen Arusha, Julai 24, 2024
Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, ukipanda kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023 hadi 5.5 mwaka 2024, hatua inayochukuliwa kuwa ishara nzuri kuelekea Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2030.
Takwimu hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Clement Sangu (Mb), alipokuwa akifunga rasmi Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala (TAPA-HR) uliofanyika jijini Arusha.
“Jitihada kubwa za serikali zimechangia ukuaji huu wa uchumi. Lakini mafanikio haya hayawezi kuendelea bila usimamizi makini wa watumishi wa umma,” alisisitiza Mhe. Sangu.
Wajibu wa Wataalamu wa Rasilimali Watu
Katika hotuba yake, Naibu Waziri Sangu aliwaasa wataalamu wa rasilimali watu kuhakikisha uwajibikaji na ufuatiliaji wa kina kwa watumishi wa umma, akionya kuwa kutowajibika kunaweza kuigharimu serikali kiasi kikubwa cha fedha.
Aliainisha tukio la mwaka 2016 ambapo taasisi moja ya umma iliwafukuza kazi watumishi 40 kinyume cha taratibu. Baada ya kufungua kesi na kushinda, serikali ililazimika kuwalipa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 40, huku mmoja wao akiwa anapaswa kulipwa zaidi ya bilioni moja.
“Haya ni madhara ya kutowajibika kwa mtu mmoja. Serikali inalazimika kulipa madeni badala ya kuendeleza miradi ya maendeleo,” alieleza kwa masikitiko.
Serikali Yapongezwa kwa Kuimarisha Mazingira ya Kazi
Naye Mwenyekiti wa TAPA-HR, Bi. Grace Meshy, aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka sera bora zinazolenga kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza motisha kwa watumishi wa umma.
“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwenye sekta ya utumishi wa umma. Mazingira ya kazi yameboreshwa, na kuna ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wataalamu wetu,” alisema Bi. Meshy.
Aidha, aliwashukuru waajiri kwa kuruhusu zaidi ya washiriki 1,000 kuhudhuria mkutano huo mkubwa, hatua ambayo inaonesha namna ambavyo taaluma ya usimamizi wa rasilimali watu inavyopewa kipaumbele nchini.
Ukuaji wa uchumi wa taifa unahitaji si tu sera nzuri, bali pia usimamizi bora wa watu wanaotekeleza sera hizo. Uongozi, uwajibikaji na uadilifu katika usimamizi wa rasilimali watu ni nguzo muhimu za maendeleo ya kweli.