Na GEOFREYSTEPHEN ,Mirerani
Sakata la uvamizi wa Mgodi wa Madini ya Tanzanite katika Kitalu C unaomilikiwa na serikali katika Mji wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoani Manyara sasa umeingia sura mpya baada ya Kampuni ya Tanzanite Exploler kukaidi maagizo yaliyotolewa na afisa mfawidhi wa madini RMO na kuomba msaada kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Kampuni ya Tanzania Exploler inayomilikiwa na Victor Mkenga na kampuni nyingine ikiwemo ya Saniniu Mining inayomilikiwa na Bilionea Saniniu Laizer na Kampuni ya Manga Gems{T] ltd inayomilikiwa na familia ya Mathias Manga zinatuhumiwa kuingia katika mgodi wa serikali wa kitalu C kinyume na sheria na kuvuna madini ya mamilioni ya pesa kupitia mtindo wa Bomu(kuchimba chini kwa chini).
Afisa Mfawidhi wa Madini Mirerani ,Mernad Msengi alisema katika kikao cha pamoja kilichofanyika wiki iliyopita na kuhudhuriwa na viongozi wa migodi yote wanaotuhukiwa kuvamia kitalu C pamoja na mchimbaji mzawa wa Kampuni ya Franone walikubaliana kufanya.
RMO alitoa maelekezo kwamba ,ufanyike upimaji wa mipaka upya kwa kuwashirikisha wataalamu pamoja na wahusika chini ya migodi hiyo lengo ni kutaka kijilidhisha kama kweli migodi hiyo iliingia kitalu C kinyemela.
Msengi alisema kikao hicho kilikuja baada ya kupata malalamiko ya maandishi kutoka kwa mbia wa kutalu C ,Kampuni ya Franone ambaye ni mwekezaji Mzawa anachimba kwa ubia na serikali kuilalamikia migodi hiyo kuwa inachimba ndani ya kitalu C kinyume na taratibu hivyo waliomba hatua kali zichukuliwe.
Alisema katika Kikao hicho wote walikubaliana timu ya wataalamu kufanya ukaguzi wenye kushirikisha pande zote ili kubaini mgodi gani uliingia katika kitalu C .
Hata hivyo licha ya makubaliano hayo ya pamoja ,uongozi wa Tanzania Exploler umeamua kuandika barua ya malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa kuonesha haikuridhika na maamuzi hayo jambo linalodhiritesha jitihada wizara ya madini kumaliza mgogoro huo.
Mmoja wa Wakurugenzi wa kampuni ya Tanzania Exploler aliyejitambulisha kwa jina la Lenganasa Soipey alipohojiwa kwa simu na kuulizwa kulikoni kushindwa kutekeleza maamuzi ya pamoja alisema kuwa kamwe hawezi kuyafuata maagizo hayo kwa kuwa ni kesi ya Nyani kwenda kwa Ngedere hivyo ameamua kwenda kazi za juu kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupata msaada zaidi.
Lenganasa Soipey alisema hawezi kukubaliana na maamuzi ya kikao hicho na kusema kuwa anaona kuwa bora akimbilie kwa Mkuu wa mkoa ambaye anaweza kuwa msaada kwake.
Kwa upande wake afisa mfawidhi wa madini ,RMO Msengi alisema ameshatoa taarifa kwa wakuu wake wa kazi kusubiri maelekezo mengine .
Alisema kwa kuwa jambo hilo limefika kwa mkuu qa mkoa hawezi kuendelea na zoezi la uhakiki wa mipaka na anasubiri maamuzi na maelekezo ya mkuu wa mkoa wa Manyara.
Awali tukio lingine liliwahi kutokea march 10 hadi 13 mwaka huu kwa kampuni ya Gem Rock Venture inayomilikiwa na mfanyabiashara Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti kuchimba kwa njia haramu katika kitalu C na kufanya serikali kukosa mapato hivyo hatua zaidi zinahitajika juu ya kuthibiti uchimbaji huo haramu kwa wafanyabiashara wakubwa.
Mkurugenzi wa Manga Gems,Brayan Manga alipoulizwa juu ya tukio hilo alijibu kwa dharau na kusema kuwa hana taarifa za kuvamia kitalu C na kusema kuwa hakuna Mtaalamu aliyethibitisha kuwa yeye amevamia mgodi huo.
Mfanyabiashara Victor Mkenga na Bilionea Saniniu Laizer hawakuweza kupatikana kuelezea tuhuma hizo kwa kuwa simu zao za kiganjani zilikuwa zikiita bila ya kupokelewa pamoja na kutumiwa ujumbe wa sms mara zote bila ya mafanikio lakini juhudi zaidi zinaendelea kuwasaka.
Ends..