Na Geofrey Stephen Arusha
WANAWAKE wameshauriwa kuondoa mfumo tegemezi unaowarudisha nyuma kinaendeleo, badala yake wajenge tabia ya udhubutu itakayosaidia kuwaimarisha kiuchumi ndani ya familia zao na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya mstaafu BETH MKWASA wakati alipohudhulia maadhimisho ya kila mwezi ya kusemezana kwa wanawake wakatoliki Tanzania (WAWATA) wa jimbo kuu katoliki la Arusha yaliyofanyika katika Parokia ya Moyo Safi wa Bikra Maria,Ungalimited jijini Arusha.
Mkwasa ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara na mwandishi wa habari Mwandamizi mstaafu, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na wanawake wengi wenye nguvu na taifa linawategemea, lakini wengi wao bado wanaishi kwa mfumo wa utegemezi.
“Kina mama waachane na mfumo wa kiafrika wa utegemezi wanaweza kujiajiri wenyewe kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo waache kuwategemea wanaume, mama anatakiwa asaidie kulea familia”
Awali Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Bikra Maria, Padri Festus Mangwangi alisema wanawake wakatoliki [WAWATA] wamekuwa na desturi ya kusemezana ili kukumbushana wajibu katika kutekeleza majukumu yao na kujiweka kando na mambo yasiyompendeza mungu.
Aidha aliwahimiza watu kupenda kwenda kwenye nyumba za ibada ili kufafanuliwa neno la mungu na jijsi gani ya kuishi ili mioyo yao iwe na hofu na mungu .
“Leo Dekania ya WAWATA jiji Mashariki yenye parokia 11 na vigango vyake ,wamekusanyika katika parokia ya moyo safi Ungalimited kwa ajili ya kusemezana na walichagua mada isemayo mama mkatoliki na imani katoliki, kuitunza, kuitetea na kuisambaza “
Alisema mwanamke anawajibu wa kushiriki maendeleo na kuhudumia familia kama shamba la mzabibu pasipo kumtegemea mwanaume .
Padri Mangwangi aliwaeleza WAWATA kuwa mwanamke anawajibu wa kushiriki shughuli za kiuchumi na kuondoa mfumo wa kiafrika wa kumtegemea mwanaume akafanye kazi.
Naye mwenyekiti wa WAWATA jimbo kuu katoliki la Arusha,Bakhita Manga alisema utaratibu wa kusemezana kwa akina mama wakatoliki kumesaidia kujenga utume wa kujitolea , malezi, kujitambua na kufundishana .
“Leo tumekutana Dekania moja kati ya nane za jimbo kuu katoliki la Arusha,kwa lengo la kusemeza a kama ilivyo desturi yetu ,kila mwaka tunakuwa na mada tatu na kila jumapili ya pili ya mwezi ni siku ya kusemezana kwa kila mwanamke mkatoliki kwa kuchagua mada mojawapo “
Alisema kupitia utaratibu huo wa kusemezana kumesaidia kuwajenga kiimani na mwanamke kutambua wajibu wake na namna ya kushiriki katika maendeleo ya kifamilia.
Mwisho