Na Geofrey Stephen , ARUSHA
CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA), kimejipanga kufanya maboresho Makubwa ili kwendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuanza kutumia madarasa mtandao ili kuwezesha kutoa elimu kwa kundi kubwa la wanafunzi maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi
Madarasa hayo ya kisasa yatamwezesha mwalimu atakayekuwa kwenye chumba cha darasa katika kampasi zake Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Babati mkoani Manyara na Songea na nchi watakazofungua matawi Sudan Kusini na Comorro kusoma kwa wakati mmoja.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka wakati alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali chuoni hapo juu ya maendeleo ya chuo hicho kilichopo Njiro nje kidogo ya jiji la Arusha.
Aidha Sedoyeka alisema katika taasisi hiyo ya uhasibu kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka sh,bilioni 12.8 kwa mwaka 2020/21 na kufikia sh,bilioni 37.8 mwaka 2023/24.
Alisema kampasi za Babati na Dodoma zimekamilika kwa sehemu kubwa, zikibaki kufanya udahili, huku akisisitiza fedha za mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi HEET) wa dola za Marekani milioni 21, zimewezesha maboresho na mabadiliko hayo, yanayokwenda kukifanya kuwa chuo kikubwa nchini kwa kuwa na miundombinu bora, wahadhiri na wanafunzi wengi.
Prof Sedoyeka alisema ongezeko la wanafunzi wanaofikia takribani 20,000 kwa sasa katika Kampasi ya Arusha kinampa matumani ya kuendelea kukipanua zaidi japo alisema lengo ni kufikisha wanafunzi 30,000.
“Mwaka 2025, chuo chetu kinatarajiwa kuwa na wanafunzi 20,000 idadi ambayo itakifanya kuwa miongoni mwa vyuo vikuu vyenye idadi kubwa ya wanafunzi nchini”
Wakati huo huo Prof Sidoyeka alisema IAA, imejipanga kuwashirikisha wataalamu kutoka nje ya nchi kutoa mafunzo ya ubunifu kwa wanafunzi ili wajue mbinu za kuanzisha viwanda kwa lengo la kuzalisha ajira.
Alisema hadi sasa wanafunzi nane wamefanikiwa kuanzisha viwanda baada ya kupata maarifa na ujuzi kutoka chuoni hapo na lengo ni kuhakikisha wanafunzi wengi wanamiliki viwanda vyao.
Alisema ubora wa mafunzo ya uhasibu, biashara, tehama, fedha , utalii na ukarimu katika mahitaji ya soko chuo hicho kinalazimikan kufungua kampasi zingine mpya kwenye mikoa ya Dodoma, Manyara na Ruvuma ili kuongeza wigo wa huduma zake .
Prof. Sedoyeka, alisema kwa sasa chuo kina watumishi 370, kati yao 32 ni wenye Shahada ya Uzamivu na wanatarajiwa kufikia 100 baada ya wengine 88 kumaliza masomo yao.
Hata hivyo chuo hicho kimetangaza mpango wa kufungua kampasi mpya nje ya nchi, moja katika Visiwa vya Comoro na nyingine Sudan Kusini , kufuatia mahitaji makubwa ya elimu ya juu na fursa za maendeleo katika maeneo hayo.
Ends..