Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kusimamia na kuwa wazalendo katika matumizi sahihi ya mitambo mipya iliyonunuliwa kwa lengo la matengenezo ya barabara za ndani ya jiji ambazo hazina viwango vya TARURA.
Mapema leo katika viwanja vya mgambo Akizindua mitambo hiyo iliyogharimu zaidi shilingi bilioni 1.7, Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amewataka watendaji hao kuhakikisha lengo linatimizwa la kuwa na barabara za ndani zenye ubora ili wananchi wafanye majukumu yao ya kulijenga taifa katika mazingira rafiki.
Hata hivyo amesisitiza suala la Madiwani na Watendaji wa mitaa kusimamia usafi wa mitaa unaofanyika kila siku ya jumamosi ili kufanya Jiji kuwa safi na kuvutia zaidi Wageni.
“Pesa iliyonunua mitambo hii imetokana na kodi za wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, kupitia usimamizi wa Madiwani nategemea mitambo hii kutunzwa vyema, hivyo natoa rai kwa yeyote kuwa mlinzi wa mitambo hii,” amesema na kuongeza:
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amepongeza hatua hiyo iliyofikiwa ambayo imefanikisha manunuzi ya Maroli 2 na Mtambo 1 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7, hatua inayopelekea kufikia lengo lililowekwa na Baraza la Madiwani.
“Licha ya manunuzi ya mitambo hii na kulipa mapato serikali kuu, bado tumebaki na chenji ambayo tutahakikisha Kata 25 za Jiji na Mitaa 154 zinanufaika kwa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa kila Kata, lengo ni kununulia vifusi ili barabara zote za mitaa ziweze kuwa imara” amefafanua Kayombo.
Diwani wa Kata ya Sokoni 1 Saruni Olodi, amepongeza jitihada za Baraza la Madiwani kwa kuokoa gharama za kukodisha mitambo, hadi kufikia hatua ya kumiliki mitambo yao wenyewe.
“Niwatoe wasiwasi wananchi wetu wawe na subira, mambo yatakaa sawa kwa kata zote ambazo zimekuwa na changamoto ya ubovu wa barabara kwa kipindi kirefu” amesema Olodi.
Mwisho .