Na Mwandishi wa Wetu KITETO.
WAKULIMA katika Kitongoji cha Napulukunya Kijiji cha Kimana wilayani Kiteto Mkoani Manyara wameiomba serikali kupitia waziri wa Ardhi , Deogratius Ndejembi kuingilia kati mgogoro wa muda mrefu unaofukuta kati yao na wafugaji kufuatia viashirio vya uvunjifu wa Amani vinavyoanza kujitokeza.
Aidha wakulima hao zaidi ya 70 wanamtuhumu mkuu wa wilaya hiyo,Remidius Mwema pamoja na Mbunge wa jimbo la kiteto,Edward Lekaita kuchochea mgogoro huo kwa kupendelea wafugaji ambao wamekuwa wakiingiza mifugo yao kwenye mashamba yao na kufanya uharibifu wa mazao bila kuchukuliwa hatua stahiki.
Wakiongea na vyombo vya habari kwa niaba ya wenzao ,Singilbert Silayo,Deogratiaus Kulaya ,Silvester Daha na Elurehema Musan wamedai kuwa eneo hilo ni eneo la asili na lililokuwa linamilikiwa na wazawa enzi za mababu na wao wamenunua kutoka kwa wazawa miaka sita iliyopita na kupatiwa hati za umiliki ila wanshangaa kuanza kufukuzwa na mkuu huyo wa wilaya bila kuwashirikisha
“Huu mgogoro haukuwepo ila umekuja kuanzishwa na kuchochewa na mkuu huyu wa wilaya baada ya kuja na utaratibu wa kuwaondoa wakulima akidai maeneo hayo ni maeneo ya makazi na sio maeneo ya kilimo, jambo ambalo sio kweli”
Wamedai kuwa mkuu huyo wa wilaya amekuwa akitumia genge la wahuni wakiwemo masai wenye sime kwenda kufanya vurugu kwenye maeneo yao jambo ambalo wakulima wamedai hawatavumilia na wamejipanga kujibu mapigo na hivyo wamemwomba waziri wa Ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi kuingilia kati sakata hilo linaloashiria uvunjifu wa amani.
Aidha wamedai kuwa moja ya uharibifu uliofanywa na watu hao wanaodaiwa kuongozwa na Mkuu huyo wa wilaya ni kufyeka mazao yao ya mahindi ambayo yalikaribia kuvunwa,wakiwa na lengo la kutaka kuwaondoa kimabavu katika maeneo yao.
Naye mkulima Elirehema Musan alisema kuwa kikundi hicho kimekamata matrekta yao ya kilimo na kukamata baadhi ya wakulima hao na kuwapeleka kituo cha polisi na kunyimwa dhamana.
“Malalamiko yetu tumeyafikisha kwa viongozi wa chama cha Mapinduzi ngazi ya wilaya na kwa mkuu wa mkoa wa Manyara lakini tumekosa majibu baada ya kujibiwa kuwa suala hilo linashughulikiwa na mkuu wa wilaya ”
Akizungumzia suala hilo,Mkuu huyo wa wilaya hiyo,Remidius Mwema alisema kuwa kijiji cha kimana kimetenga eneo la Napulukunya kwa ajili ya makazi nasio shughuli za malisho wala kilimo na kuwataka wananchi walio vamia eneo hilo kuondoka.
“Eneo la Napulukunya ni eneo lililotengea kwa shughuli za Makazi na nyaraka zipo lakini kuna watu wanafanya shughuli za kilimo na tumefanya jitihada za kukutana nao na kuwaelimisha ila watu wao wamefanya ukaidi na kuendelea kulima kinyume cha utaratibu”
“Watu wao wamevamia maeneo hayo na kujimilikisha kinyume cha sheria,kuna mtu anaekari miasaba ,kuna mtu anaekari miambili na kuna baadhi ya viongozi wamewapatia kinyume cha utaratibu, kwa sasa tunapambana na watu ambao wamekaidi kuondoka”
Alisisitiza kuwa hao watu ni wavamizi lazima waondoke na hizo tuhuma wanazosema kuwa nimehongwa na wafugaji sio za kweli njooni nitawaonesha vielelezo kuhusu huo mgogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Qeen Sendiga alipohojiwa alisema kuwa suala hilo linahusu ngazi ya wilaya na yeye bado hajalipata na kuelekeza kuwa ni vizuri watu hao wakawasiliana na mkuu wa wilaya .
Naye mbunge wa jimbo la Kiteto, Edward Lekaita alipoulizwa kuhusiana na madai ya wananchi hao alisema kuwa yeye hana mamlaka ya kuwaondoa wananchi katika ardhi yao.
“Mimi ni mbunge sina mamlaka ya kumpa mtu Ardhi ama kumwondoa hizo ni siasa zenye nia ya kunichafua ukizingatia mwaka huu ni uchaguzi”
Alisisitiza kuwa hajawahi kushiriki mpango huo wa kuhujumu wananchi wake hasa wakulima na kupendelea wafugaji kwa sababu anatoka katika jamii ya kifugaji.
Ends..