Na Geofrey Stephen Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kufungua Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii wa vyakula la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika lililoanza leo Aprili 22, 2025 jijini Arusha.
Aidha jukwaa hilo linatarajia kukutanisha washiriki takribani 300 wakijumuisha viongozi waandamizi katika sekta ya utalii na ukarimu, watumishi wa serikali, pamoja na wataalamu wa masuala ya upishi kutoka ndani na nje ya Afrika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha leo.
Amefafanua kuwa ufunguzi wa Jukwaa hilo utafanyika April 23, 2025,ambapo kupitia jukwaa hilo la kihistoria Tanzania itapata fursa ya kuonesha utajiri wa vyakula vya asili vinavyotokana na makabila zaidi ya 120 nchini Tanzania.
“Tukio hili linalenga kuangazia uhusiano muhimu kati ya utamaduni wa upishi na utalii, pamoja na kufanya tathmini ya mchango wa utalii wa vyakula katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, kuhifadhi urithi wa kiutamaduni, na kuboresha maisha ya jamii linaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), pamoja na Basque Culinary Center” amesema Mhe. Chana.
Amesema kuwa,jukwaa hili litakuwa ni sehemu mahsusi ya kukuza utalii wa chakula, na hivyo kuongeza wigo wa mazao ya utalii nchini, kuwezesha wageni kukaa muda mrefu zaidi nchini na kuchochea mchango wa utalii katika uchumi wa Taifa letu.
Aidha Waziri Chana ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wote wa sekta ya utalii na mapishi, pamoja na wananchi wote, kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono na kuendeleza dhana hiyo muhimu ya utalii wa vyakula, kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta ya utalii na utambulisho wa Taifa letu kimataifa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Shirika la Utalii Duniani, Elcia Grandcourt, amesema jukwaa la kimataifa la utalii wa vyakula litasaidia kukuza utalii hasa vijijini na kuhifadhi utamaduni wa asili.
“Hii ni nafasi yetu ya kuonyesha tunachoweza kutoa sio tu kutoka Tanzania bali katika Bara lenyewe la Afrika” amesema Bi. Grandcourt.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa kimataifa wakiwemo Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani, Bw. Zurab Pololikashvili, pamoja na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Dkt. Auxillia C. Mnangagwa.
Mwisho.