Na Mwandishi wa A24Tv
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara upande wa Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Kitovu cha teknolojia za zana za kilimo kitakachoanzishwa Wilaya ya Maswa kitaongeza tija ya uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo kuanzia maandalizi ya shamba, uvunaji na uchakataji wa mazao hayo.
Dkt Hashil ameyasema hayo Juni 4, 2022 alipotembelea Jengo la raslimali za kilimo lililopo kijiji cha Mwandete Wilaya ya Maswa litakalotolewa kwa Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini (CAMARTEC) kwa ajili ya kuanzisha Kitovu cha teknolojia za Kihandisi kitakachotoa huduma za mafunzo na zana za kilimo wilayani humo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw . Simon Berege amesema Halmashauri hiyo iko katika makubaliano na CAMARTEC kuanzisha kitovu hicho cha teknolojia za kihandisi ambacho kitaongeza tija katika mazao ya kilimo hasa mazao yanayotoa malighafi viwandani ikiwemo Pamba na alizeti katika wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema halmashauri yake iko tayali kuwawezesha wakulima kupata zana hizo kwa mikopo yenye riba nafuu kupitia mifuko mbalimbali ili waweze kupata zana hizo na kuzitumia katika shughili zao za kilimo na hatimaye kuongeza tija katika nazao yao, ajira na kipato.
Aidha akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya sekta ya Viwanda na biashara kwa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi huyo amesema Wilaya hadi sasa ina viwanda vikubwa 5, vya kati 3 na vidogo vidogo 204. Kati ya Viwanda hivyo Halimashauri inamiliki Kiwanda cha kusindika unga wa viazi lishe, Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi na Kiwanda cha kukoboa mpunga na kupanga madaraja ya mchele.
Kaimu Mkurugenzi wa CAMARTEC Mhandisi Pythias Ntella akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Mwandete Wilaya Maswa ujio wa kitovu cha zana za kilimo kitakachoongeza tija katika mazao yao kwa kutumia zana zenye teknolojoa rahisi Juni 4 2022.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa CAMARTEC Mhandisi Pythias Ntella Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kutoa mafunzo na kuunda mashine ambazo zinahitajika katika maeneo hayo hasa zana za maandalizi ya shamba kama trekta, mashine za kupura alizeti na mtama, mashine za kukata na kufunga malisho ya mifugo, mashine za vipandio na nyingine nyingi kulingana na mahitaji halisi ya wakulima na wafugaji mkoani humo na mikoa yote kwa ujumla.