Na Mwandishi wa A24Tv Geita .
Kamishna wa Tume ya Madini Janet Lekashingo amewataka watanzania kujitokeza kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini kutokana na kuwepo kwa fursa mbalimbali kwenye mnyoyoro wa madini kuanzia uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini na utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
Lekashingo ameyasema hayo kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha TBC1 leo tarehe 08 Oktoba, 2022 kwenye Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika Viwanja vya Bombambili mjini Geita.
Amesema ili kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na Sekta ya Madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ili wananchi waweze kupata fursa za ajira na kutoa huduma mbalimbali kama vile vyakula, ulinzi na ajira kwenye migodi ya madini.
Katika hatua nyingine, amewataka watanzania kuanzisha viwanda vya kutengeneza vipuri na huduma za usafiri kwenye migodi ya madini, biashara ambayo itakuwa ni endelevu hata mara baada ya kumalizika kwa uchimbaji wa madini.
“ Zipo kampuni zinazomilikiwa na watanzania kama Blue Coast kwa ajili ya kutoa huduma za vifaa na usafiri kwenye migodi ya madini, mfano ambao ni mzuri; tunaomba wadau wengi zaidi kujitokeza ili kunufaika kwa kuwa na biashara endelevu,” amesisitiza Lekashingo.
Awali akielezea maonesho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara amesema kuwa maonesho yamekuwa na mafanikio makubwa kwani yametumika kama fursa kwa kampuni kubwa za uchimbaji wa madini kutoa elimu ya teknolojia mpya ya uchimbaji wa madini na wananchi wengi kupata elimu kuhusu taratibu za kupata leseni za uchimbaji na biashara ya madini kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Aidha, amesema kuwa kupitia maonesho husika wachimbaji wadogo wamepata nafasi ya kujifunza teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchenjuaji wa madini pasipo kuathiri mazingira.