Moses Mashalla,Arusha
Mfanyabiashara wa madini ya vito ambaye aliwahi kutajwa kuwa bilionea wa madini aina ya Spinner,Salim Alaudin maarufu kama “Salim Almasi” amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kukutana na wafanyabiashara wa sekta ya madini nchini ili waweze kumweleza changamoto wanazopitia.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ulanga ametoa kauli hiyo wakati akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari Mfanyabiashara huyo amesema kwamba Rais Samia ni vyema akaitisha kikao na wadau wa sekta ya madini nchini kama ambavyo anakutana na makundi mbalimbali ndani ya jamii.
“Rais Samia ni vyema akutane na wadau wa sekta ya madini ili tuweze kumshauri na kumweleza masuala mbalimbali kama changamoto tunazopitia “amesema Alaudin.
Hatahivyo,amesema kwamba serikali ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki hususani katika usafirishaji wa madini mbalimbali nje ya nchi kwa kuwa wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali.
Hatahivyo,Mfanyabiashara huyo amesema kwamba ana matarajio ya kuanzisha utalii wa madini katika eneo lake la mgodi wilayani Mahenge kama njia mojawapo ya kuwavutia watalii nchini.
Mfanyabiashara huyo amesema kwamba katika eneo hilo tayari amejenga nyumba ya kifahari kwa ajili ya watu kufikia ambapo wageni mbalimbali watapata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika mgodini hapo jambo ambalo litachangia kukuza sekta ya utalii nchini.
Amesisitiza kuwa anatarajia kununua usafiri wa ndege aina ya helicopter ambayo itarahisisha usafiri kwa watu wanaotembelea eneo hilo ambapo pia wanafunzi wa shule mbalimbali watapata fursa ya kujifunza shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika eneo hilo.
“Matarajio yangu makubwa ni kuona watanzania wanavaa madini yao wenyewe hata kama kwa gharama ndogo na sio wageni pekee “amesema Mfanyabiashara huyo.
Mwisho