_Ni kupitia ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, uboreshaji wa huduma za jamii unaofanywa na migodi ya madini_
*KAHAMA*
Watoa huduma kwenye migodi ya madini katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga wameipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini hali iliyopelekea watanzania wengi kushiriki katika sekta hiyo kupitia utoaji wa huduma katika shughuli za uchimbaji wa madini na kuongezeka kwa kasi ya uboreshaji wa huduma za jamii unaofanywa na kampuni za madini.
Watoa huduma hao waliyazungumza hayo jana tarehe 29 Novemba, 2022 katika eneo la Kahama kwenye mahojiano ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii.
Walieleza kuwa kupitia usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini manufaa mengi yameonekana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa fursa za utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini kama vile usafirishaji, ukarabati wa mitambo, ulinzi na uboreshaji wa huduma za jamii hususan katika maeneo ya afya na elimu.
Mkurugenzi wa kampuni inayojihusisha na ukarabati wa mitambo na ujenzi ya Mjasilia Group Company Limited, Hamis Shaban alisema kuwa kuanzishwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini kulipelekea binafsi kuachana na ajira na kuamua kuanzisha kampuni binafsi ambayo imekuwa ikitoa huduma katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick- Bulyanhulu ambapo mpaka sasa ametoa ajira kwa wataalam 46 wanaotoka katika maeneo ya vijiji vya jirani katika mgodi huo.
Aliwataka watoa huduma wengine nchini kuchangamkia fursa zinazotangazwa na kampuni za uchimbaji wa madini nchini na kutoa huduma kwa uaminifu mkubwa na kujipatia kipato sambamba na kutoa huduma kwa jamii inayowazunguka.
Naye mmiliki wa kampuni ya usafirishaji inayotoa huduma katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick- Bulyanhulu, ya FRESTER, Fredy Shoo akielezea mafanikio yake tangu alipoanza kutoa huduma katika mgodi huo alieleza kuwa amefanikiwa kuongeza mabasi kutoka moja hadi mabasi 75 ambayo yanatoa huduma nchini ambapo yanasimamiwa na watumishi 300 aliowaajiri.
“Ninachukua fursa hii kutoa shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Madini kupitia uboreshaji wa kanuni za madini zenye lengo la kuhakikisha watanzania wananufaika kupitia utoaji huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na Tume ya Madini kwa kusimamia kwa karibu kanuni na sisi kuendelea kunufaika,” alisema Shoo
Akielezea namna elimu ilivyoboreshwa katika eneo la Nyang’hwale mkoani Geita, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Kharumwa, Justine Mathias alieleza kuwa shule hiyo ilijengwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick-Bulyanhulu baada ya kukubaliana na halmashauri na kuanzishwa mapema Machi mwaka huu, ambayo itakuwa mkombozi wa elimu kwa wananchi wanoishi jirani na eneo hilo.
Sambamba na kuushukuru Mgodi wa Barrick kwa ujenzi wa shule hiyo, aliongeza kuwa uongozi wa shule upo katika mkakati wa kuendelea kujenga majengo mengine na kuboresha mazingira ya elimu kwa kuongeza walimu waliobobea na kujenga msingi utakaowawezesha wanafunzi kuendelea katika masomo ya elimu ya juu mbeleni na kuweza kushindana na soko la ajira kimataifa.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Bugarama kilichojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick- Bulyanhulu kilichopo katika eneo la Msalala mkoani Shinyanga, Dkt. Beatha Alistides aliongeza kuwa, tangu kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho na kuanza kazi rasmi idadi ya vifo imepungua kutokana na kuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 40,000 tofauti na awali ambapo walikuwa na kituo kidogo kilichokuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 2000 tu.
“ Niishukuru Serikali kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini kwa kuhakikisha migodi ya madini inaboresha huduma kwa jamii, mfano mzuri ni Mgodi wa Barrick ambao kwa kiasi kikubwa umeokoa maisha ya wanachi hasa wakinamama wajawazito,” alisisitiza Dkt. Alistides.
Awali akielezea namna mgodi wa Barrick unavyotekeleza kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na uboreshaji wa huduma za jamii, Mrakibu wa Mahusiano ya Jamii ya Mgodi huo, Zuwena Senkondo sambamba na kupongeza Serikali kwa usimamizi wa kanuni hizo alifafanua kuwa mgodi umeendelea kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja ujenzi wa mabweni ya wasichana, uanzishwaji wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Kharumwa, ujenzi wa kituo cha afya cha Bugarama n.k.
“Tunashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa ambao tumekuwa tukipata kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini, tutaendelea kuboresha huduma za jamii sambamba na kutoa fursa kwa watanzania kwenye shughuli za mgodi; katika mwaka huu wa 2022 tumetenga shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii, alisisitiza Senkondo