Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT ) kimetakiwa kusimamia ubora wa elimu inayotolewa chuoni hapo ili kuhakikisha hadhi ya Chuo na elimu ya Tanzania kwa ujumla inalindwa.
Hayo yamesemwa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango wakati alipotembelea Chuo hicho kwa lengo la kukutana na viongozi, wanataaluma na watumishi ili kujionea hali halisi ya chuo hicho ambapo amesema kumekuwa na malalamiko kidogo kuwa kuna urahisi wa kuhitimu katika chuo hicho hivyo kuonekana baadhi ya wahitimu kutokuwa na ubora.
“Kuna malalamiko kuwa baadhi ya wahitimu wa Shahada za Uzamili na Uzamivu huandikiwa ripoti zao za utafiti na hivyo kusababisha kuajiriwa watu wasio na uwezo kulingana na vyeti vyao. Nawaagiza Waziri wa Elimu, Makamu Mkuu wa Chuo na Wasaidizi wako mfuatilie hilo na kuwachukulia hatua watakaobainika kuandikiwa,” amefafanua Dkt. Mpango.
Mhe. Mpango amepongeza OUT kwa utoaji wa elimu masafa mfumo ambao unasaidia sana hususan wakati chuo kina changamoto ya majengo na upungufu wa wahadhiri. Aidha amewahimiza Watanzania kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na chuo kusoma kupitia elimu masafa.
“Nipongeze sana mpango huu na niseme dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kutatua changamoto zilizopo, kwa namna ya pekee Waziri wa Elimu ningependa kuona mpango mahsusi wa kuandaa Wahadhiri na hasa kwa ajili ya mafunzo kwa wenye ulemavu na uwepo wa vifaa,” ameongeza Dkt. Mpango
Akiongea katika ziara hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema katika mageuzi makubwa ya Elimu yanayokuja suala mojawapo litakuwa ni ajira za Wahadhiri wa Vyuo Vikuu..
“Zamani ilikuwa mwanafunzi anaefanya vizuri kwa kupata GPA nzuri ndio anachukuliwa kuajiriwa lakini katika Sera mpya ya Elimu hilo tutalishughulikia kuhakikisha kwamba ajira ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu inaendana na kwingineko duniani. Tutaajiri mtu kwa kumpima na sio kwa kuangalia GPA pekee,” amesema Waziri Mkenda.
Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kipaumbele katika elimu na kwa Elimu ya Juu imeongeza fursa kwa kuongeza mikopo kutoka Shilingi bilioni 464 hadi kufikia bilioni 654.
“Serikali imeongeza fedha za mikopo ya Elimu ya Juu , kazi kubwa tuliyo nayo ni kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa haki na kwa kufuata vigezo vilivyowekwa,” ameongeza Waziri Mkenda.
Ameongeza kuwa Wizara kupitia Mradi wa HEET inaendelea kuongeza fursa za elimu ya juu kwa kujenga kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 ikiwemo Kigoma, Lindi, Mtwara, Tabora, Tanga na Kagera.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha OUT, Profesa Elifas Bisanda ameishukuru Wizara ya Elimu na Serikali kwa kuwajengea majengo yaliyogharimu zaidi ya Shilingi bilioni mbili katika mikoa ya Simiyu, Geita, Kigoma, Lindi na Manyara.
Ameongeza kuwa Wizara kupitia Mradi wa HEET imekitengea chuo hicho Dola milioni 9 ambazo zitatumika kujenga maabara 7 za kisayansi katika Kanda mbalimbali pamoja na kusomesha baadhi ya wanataaluma katika ngazi ya Umahiri na Uzamivu na kuahidi kutumia fedha hizo kwa umakini ili kuleta tija.