Doreen Aloyce , Dodoma
KATIKA kuboresha sekta ya usafiri majini Shirika la Uwakala wa meli Tanzania (TASAC) imeweza Kuunda nyenzo za udhibiti wa huduma za usafiri kwa njia ya maji pamoja na kukamilisha mradi wa kimataifa wa mawasiliano na uchukuzi katika Ziwa Victoria ambao utagharimu bilioni 59.23.
Akizungumza na vyombo vya Habari jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa Majukumu wa shirika hilo kwa awamu ya sita Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Mkeyenge amesema tangu kuanzishwa kwake inajivunia mambo mengi sana hususan juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya maji.
Amesema, mradi huo unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda utagharimu kiasi cha Shilingi 59.23 Bilioni, ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni Shilingi 19.97 Bilioni zikijumuisha gharama za kazi za ndani.
Vituo hivyo, vitasaidia kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia maji na katika uokozi majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria
Aidha amesema shirika la wakala wa meli Tanzania umeendelea kuimarisha miundo mbinu ya mfumo wa Tehama ikiwemo ambazo zinasaidia kukusanya mapato na huduma za biashara ya meli.
Katika hatua nyingine Shirika limeshiriki kuongeza mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka kutoka Shilingi Bilioni 9.1 katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi kufikia Shilingi Bilioni 43.5 katika mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 21 na hivyo kufanya jumla ya mchango wa TASAC katika mfuko mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne kuwa Shilingi Bilioni 104.5.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, TASAC tangu kuanzishwa kwake 2019 inajivunia juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri majini ikiwa ni pamoja na Kukagua meli za nje zinazofika katika bandari zetu
“kwa mujibu wa Makubaliano ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean Memorandum of Understanding – IOMOU) ambayo Tanzania ni mwanachama,Katika utekelezaji wa hili TASAC tumekagua meli za kigeni 36 kwa kipindi kuanzia julai 2022 hadi desemba 2022, na kuanzia Januari 2023 tumekagua meli za kigeni 37 ambapo tunategemea kukagua meli 61 hadi kufikia juni 2023”.Alisema Mkeyenge
Akiendelea kutaja mafanikio mengine ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Mkurugenzihuyo amesema TASAC imeanza majadiliano ya kuingia katika makubaliano (Memorandum of Understanding MoUs) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia ili kufungua fursa za ajira kwa mabaharia nchini ambapo nchi 19 ikiwemo Panama, Malta, Cyprus, Qatar, Korea, Ghana pamoja na Jamhuri ya Watu wa China.
“Mazungumzo yapo katika hatua mbalimbali na yanaendelea vizuri kwa baadhi ya nchi kwa mfano Qatar tayari wameshakubali na tunatarajia kuwekeana saini muda wowote kuanzia sasa”Alieleza
Amesema TASAC imewajengea uwezo maafisa 42 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kuhusu uratibu wa utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Dharura katika kukabiliana na umwagikaji wa mafuta baharini (National Maritime Oil Spill Response Contingency Plan NMOSRCP).
“katika kutekeleza hili TASAC imeendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa wetu, hususan wanaofanya kaguzi kwa vyombo vya kigeni vinavyoingia katika bandari zetu Port State Control (PSC) ambapo kwa kipindi cha kuanzia julai 2022 hadi Februari 2023, maafisa 11 wamepata mafunzo hayo,na kufikia juni 2023 maafisa wengine 6 watapata mafunzo hayo, 3 katika nchi ya Italia na 3 katika nchi ya Bangladeshi”.Alifafanua
Ikumbukwe kuwa TASAC ilianzishwa chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake Februari, 2018 iliyokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hususan kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuinua mchango wa usafiri kwa njia ya maji.