Mwandishi wetu wa A24Tv .Babati.Ongezeko la matukio ya ujangili wa Twiga na uvamizi katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge sasa litaanza kushughulikiwa kwa mbinu mpya kwa ushirikiano wa vyombo vya Dola,Wanasheria na Askari wa Burunge WMA.
Matukio ya ujangili wa Twiga,ukataji miti na uvamizi maeneo yaliyohifadhiwa yameongezeka katika eneo hilo ambapo hivi karibuni watu wawili walikamatwa kwa tuhuma za mauwaji ya Twiga ili kufanya biashara ya nyama.
Burunge WMA ni eneo la hifadhi lililopo katikati ya hifadhi za Taifa za Manyara na Tarangire likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 283 likiundwa na Vijiji 10 na licha ya kukamatwa watuhumiwa kadhaa wa ujangili wamekuwa wakiachiwa kutokana na mapungufu katika ukamataji.
Mkuu wa upelelezi mkoa Manyara (RCO) Juma Majura akizungumza na askari wa Burunge WMA alisema ni lazima uwepo ushirikiano mzuri wa vyombo vya Dola Ili kukabiliana na ujangili.
Majura alisema polisi mkoa Manyara ipo tayari kutoa ushirikiano na askari wa hifadhi hiyo, wanasheria na ofisi ya Mashitaka Ili kuhakikisha unakuwepo ulinzi wa Wanyamapori.
Wakitoa mafunzo kwa askari wa Burunge WMA na askari wa Wanyamapori halmashauri ya Babati,yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) Mwendesha mashitaka wa TAWA, Getrude Kariongi na mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka(DPP) mkoa wa Manyara, Blandina Msawa waliwataka askari hao, kufanya kazi kwa weledi.
Kariongi alisema kama askari hao wakikamata wa majangili na kufanya upekuzi vizuri na kuhifadhi vizuri ushahidi kesi za ujangili zitasikilizwa kwa wakati na hukumu kutolewa.
Msawa aliwataka askari hao, kuzingatia sheria katika ukamataji, upelelezi na upekuzi ili kurahisisha mwenendo wa kesi za ujangili katika maeneo yao.
Awali Afisa Mhifadhi kutoka TAWA Kanda ya kaskazini, Emmanuel Pius amesema TAWA imetoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Taasisi ya Chem Chem association ambayo imewekeza katika eneo hilo ili kuwaongezea ujuzi askari kukabiliana na ujangili.
Alisema mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kukamata,kupeleleza,kufanya upekuzi na kuhifadhi Nyara za serikali.
” Watapatiwa elimu hii askari wote wanaofanya kazi hapa Burunge na Idara za upelelezi na mshitaka Ili waweze pia kiwa na uwezo wa kutoa ushahidi mahakamani na hivyo, kurahisisha usikilizwaji wa kesi”alisema
Mkurugenzi wa Taasisi ya Chem chem na EBN ambazo zinaendesha shughuli za Utalii katika eneo hilo, Nicolas Negri alisema ili kuendeleza uhifadhi na kupambana na ujangili wataendelea kuchangia rasilimali za kutosha.
Akizungumza kwa niaba ya Negri,Meneja Mkuu wa taasisi hizo, Clever Zulu alisema ufadhili wa mafunzo kwa askari kujengewa uwezo wa upelelezi,upekuzi na ukamataji majangili Ili kufanikisha kesi ni sehemu tu ya mchango wa taasisi hiyo.
“Tutashirikiana na polisi, Ofisi ya Mashitaka mkoa Manyara,ofisni ya Mkuu wa mkoa ,Mkuu wa wilaya na halmashauri kuhakikisha rasilimali zilizopo Burunge zinatinzwa kwa manufaa ya Sasa na vizazi vijavyo”alisema
Mwisho