Na Emmanuel Octavian
Njombe
Jumla ya madai 796 ya kesi mbalimbali yameripotiwa kwa mawakili mbalimbali wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC na kupatiwa msaada wa kisheria pasina malipo yoyote huku migogoro ya ardhi ikiwa kinara mkoani Njombe.
Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na haki za binadamu Anna Henga amesema licha ya wanawake wengi kukumbwa na mikasa mbalimbali ikiwemo ya kupokwa ardhi,kukatiliwa na kunyimwa haki mbalimbali lakini idadi yao katika kuripoti madai yao imekuwa ndogo ukilinganisha na wanaume.
Henga ametoa ripoti hiyo mkoani Njombe wakati wa kufunga maadhimisho ya miaka 27 ya kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1995 ambapo mfumo dume ungali unaripotiwa katika jamii.
Wananchi mkoani Njombe akiwemo Richard Mligo na Dorcas Siame ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa sekondari wa club za haki za binadamu wanasema migogoro mingi katika jamii inachagizwa na kukosekana kwa msaada wa kisheria na gharama kubwa za kutafuta mawakili.
Katibu mkuu wizara ya Katiba na Sheria Mery Makondo kwa niaba ya Waziri wa katiba na sheria anakiri kuwapo kwa changamoto kubwa ya kucheleweshwa kwa haki kwa wananchi na kwamba serikali imeliona suala hilo na kuanza kulifanyia kazi.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga anasema wananchi wengi wanafungwa jela kwa kukosa msaada wa kisheria hivyo kituo cha sheria na haki za binadamu kiwe mkombozi kwao kupitia vituo vya msaada wa kisheria.[Paralegal].
Kutokana na kukithiri kwa migogoro mingi ya ardhi nchini Katibu tawala mkoa wa Njombe Bi.Judica Omary anasema serikali imeanzisha ofisi za ardhi kila halmashauri ili kukabiliana na tatizo hilo.
Mwaka 1995 kituo cha sheria na haki za binadamu kilianzishwa kikishughulikia changamoto mbalimbali za kukosekana kwa haki za binadamu zinazosababisha ukatili katika jamii.