Na Emmanuel mkulu
Njombe
Serikali chini ya wizara ya Maliasili na utalii nchini Tanzania imetangaza rasmi mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta ya utalii inayochangia pato la taifa kwa asilimia 17.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa kutangaza utalii kusini mwa Tanzania Waziri wa maliasili na utalii Balozi Dokta Pindi Chana akiwa mkoani Njombe amesema wizara imeweka wazi mikakati mbalimbali ikiwemo kutangaza utalii kusini mwa nchi,Utamaduni,pamoja na fursa za utalii zilizopo katika mikoa husika.
Wabunge wa majimbo ya Makambako Deo Sanga,Ludewa Joseph Kamonga na Makete Festo Sanga Wamesema ili fursa ya utalii kusini mwa Tanzania iweze kufanikiwa kwa akali kubwa kunahitajika kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara,Viwanja vya ndege pamoja na kuendeleza mambo ya asili yaliyopo.
Awali mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka amesema ifike wakati baridi iliyopo Njombe iwe fursa kwa kuwaingizia kipato wananchi na taifa ikiwa njia moja wapo ya kuutangaza utalii nchini kauli iliyoungwa mkono na Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainabu Teleck kwa niaba ya wakuu wa mikoa tisa ya kusini mwa Tanzania.
Baadhi ya wananchi mkoani Njombe akiwemo Adili Nguhula na Dokta Florian Mtei mdau wa Utalii nchini wamekiri kuwa mpango huo utakwenda kusisimua utalii kusini mwa Tanzania.