Maaskofu na wachungaji watakiwa kuwa na msimamo mmoja katika kupinga maswala ya ushoga .
Na Geofrey Stephen Arusha
Arusha.Maskofu pamoja na wachungaji wa makanisa mbalimbali yanayopinga ushoga wametakiwa kuwa na msimamo mmoja katika kupinga maswala hayo sambamba na kukataa mahusiano kabisa na makanisa yanayounga mkono maswala ya ushoga.
Hayo yalisemwa jijini Arusha na Askofu wa kanisa la kilutheri Afrika ya Mashariki (KKAM) jimbo la Arusha Mashariki ,Dk Philemon Mollel wakati akizungumza katika ibada maalumu ya kuwasimika kazini wachungaji na mashemasi.
Dk.Mollel alisema kuwa,ni lazima maaskofu na wachungaji wawe na msimamo mmoja katika kukemea vitendo hivyo vya ndoa za jinsia moja ambazo zinaungwa mkono na baadhi ya makanisa sambamba na kukataa mahusiano na makanisa hayo ,kwani ni laana kubwa na inaipeleka nchi sehemu ngumu sana.
“Katika dhana hizi ambazo tunaishi kuna makanisa ambayo kuna wachungaji mashoga na waumini mashoga na huku tunapoelekea sasa hivi ni bapaya sana kwani kwa mtindo huu ukristo unaenda kukosa nguvu kabisa hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha anasimama katika nafasi hii kukemea vikali swala hilo”alisema .
Aidha alisema kuwa,hali kwa sasa hivi imekuwa mbaya na vijana wetu wanapotea wote ni jukumu la kila mmoja kuiombea nchi na mabadiliko yanayoendelea hivi sasa kwani kuna viashiria kwamba ukristo upo mashakani kupotea na kila mmoja anatakiwa kutambua kuwa ushoga hauna toba.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuwajibika katika makuzi ya watoto wao kwani wamekuwa bize na shughuli za maisha na kuwaachia jukumu hilo watu wengine wakiwemo wasichana wa kazi za ndani jambo ambalo aliwataka kuwa makini kwani dunia ya sasa hivi imebadilika haitakiwi kumwamini mtu yoyote.
Naye Msaidizi wa Askofu wa kanisa hilo,Dk Philemon Mollel (Monaban) aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kuzungumza na watoto wao kwani vijana wengi wanaingia kwenye vitendo vya ushoga wakiwa na umri mdogo kutokana na tamaa mbalimbali za fedha .
Aidha alilitaka kanisa kuwa mstari wa mbele kukemea na kupinga ushoga huku wakimwomba Mungu atunusuru na laana hiyo kwani tunapoelekea ni pabaya sana na vitendo vinavyoendelea ni chukizo kubwa mbele za Mungu .
“Tunawaomba wachungaji mliosimikwa kazini leo mkaanze na jambo hilo kwenye makanisani wala msiogope kuzungumzia swala hilo kwani hali imekuwa mbaya sana na hatujui tunapoelekea. “alisema .
Naye Mmoja wa wachungaji waliosimikwa kazini ,Mchungaji Pendael Yohanes alisema kuwa, kanisa lina wajibu mkubwa wa kukemea swala la maadili kwani kwa sasa hivi maadili yameporomoka sana na kanisa ndo lina nafasi kubwa ya kuzungumza na waumini wake kuhakikisha maadili yanafuatwa.
Mwisho.