Na Geofrey Stephen Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, ameongoza wananchi na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo katika kampeni maalum ya usafi wa mazingira na upandaji miti Kata ya Ambureni, Halmashauri ya Meru. Tukio ambalo limefanyika leo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa.
Katika kampeni hiyo, Mhe. Makonda amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi ili kusaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Leo nina furaha kwa kwasababu tunazindua kampeni, tunapanda miti, na ninafuha kwasababu ninasherekea siku yangu ya kuzaliwa”.Amesema.
Kampeni hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, watumishi wa umma, wanafunzi, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha, ambapo miti 1,200 imepandwa katika eneo la bustani ya barabara ya Moshi Arusha.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika juhudi za kutunza mazingira kwa kufanya usafi mara kwa mara na kupanda miti zaidi ili kuimarisha mazingira na kuboresha hali ya hewa.
Kwa hatua hii, Mkoa wa Arusha unaendelea kujiimarisha kama moja ya miji inayopambana na uchafuzi wa mazingira huku ikihimiza maendeleo endelevu yanayozingatia utunzaji wa rasilimali asili.
Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini,Baraka Ladsilaus alisema benki hiyo imekuwa na kampeni ya utunzaji wa mazingira na mwaka jana 2024 benki hiyo ilipanda miti 1000 ikiwa ni hatua moja wapo ya kuifanya Arusha ya kijani.
“Leo tumeungana na mkuu wa mkoa katika zoezi la upandaji miti na sisi kama NMB tulianza kampeni hii mwaka jana kwa kupanda miti 1000 , NMB ni wadau wakubwa wa mazingira licha ya kutoa misaasa mingi mashuleni tutahakikisha tunaunga mkono utunzaji wa mazingira”
Alisema Benki hiyo imeitikia wito wa mkuu wa mkoa kushiriki zoezi hilo na wao kama taasisi za fedha watahakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali katika suala la kupanda miti na kutunza mazingira.
Alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa wazo hilo la upandaji wa miti na kuomba kuwa zoezi hilo liwe endelevu na wao wataendelea kuunga mkono bunifu za mkuu wa mkoa zenye tija li kuhakikisha Arusha inakuwa ya kijani.
Mwosho .