Na Mwandishi wa A24Tv .
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amewakaribisha wawekezaji wenye nia kutoka India kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali hususani viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba, uchumi wa bluu na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo kama Parachichi na Mbaazi zinazohitajika kwa wingi katika soko la India.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na India na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kijaji amemhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania iko tayari kupokea wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya Anga, Utalii, kilimo na Afya hususan katika viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama za uagizaji dawa nje ya nchi.
Aidha, amemshukuru Balozi huyo wa India kwa upatikanaji wa soko la mbaazi za Tanzania tani 200000 nchini India na kushauri wawekezaji kitoka nchini himo kija kiwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani katika mazao ya kilimo ambayo husafirishwa zaidi katika nchi hiyo ikiwemo Mbaazi na Parachichi ili kuongeza ajira na pato la Taifa pamoja na kuhakikisha soko la mazao hayo linalotabirika
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) na Balozi wa India nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan wakipeana mikono baada ya mazungumzo ya kuhusu kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na India na Machi 27, 2023 katika Ofisi ndogo ya Wizara, jijini Dar es Salaam. India imetoa soko la Mbaazi tani 200000 kutoka Tanzania.
Naye Balozi wa India nchini Tanzania
Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema India imekuwa na uhusiano mzuri wa Kibiashara na uwekezaji na Tanzania hususani katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo, huduma za benki, madini na afya.
Aidha, Balozi huyo amesisitiza kuwa India itaendelea kushirikiana na kuendeleza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizo pamoja na kuwaunganisha wawekezaji wa Tanzania na India kufanya biashara pamoja kupitia makubaliana ya kibiashara yaliyopo na maonyesho mbalimbali yakiwemo maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayojulikana kama sabasaba.