Na. Salim Bitchuka
Imeelezwa kuwa muamko mdogo wa vijana katika fani ya ubaharia ndio chanzo kinachopelekea taifa la Tanzania kutokuwa na Mabaharia Vijana wa kutosha.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na mkurugenzi wa huduma za Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Rajabu Mabamba wakati wa hitimisho la mafunzo kwa walimu wa Mabaharia nchini
Akimuwakilisha mkurugenzi wa TASAC, Mabamba alisema muamko umekuwa ni mdogo kwa vijana kutokana na kukosa kutengenezewa ufahamu wa kutosha kuhusu fursa zipatikanazo katika eneo hilo.
“Kwa kutambua kuwa nchi kama nchi wakati tukielekea uchumi wa Buluu kwa kushikiana na DMO tuligundua kwamba kulikuwa na upungufu katika wataalam wakutosha na kupitia mafunzo haya tutaweza kupata wataalam watakaoweza kufanya kazi ndani na hata kwenye nchi nyingine kiushindani” alisema Rajabu Mosses Mabamba.
Aidha Mkurugenzi huyo wa huduma za shirika la TASAC alisema kuhitimishwa kwa mafunzo hayo kutawezesha kupata wataalamu wa ndani ambao wataweza kutoa elimu kwa Watanzania wengi ambao wapo kwenye fani ya ubaharia na kuweza kunufaika.
Sambamba na hayo Mabamba ametumia fursa hiyo kuwahimiza vijana kujiunga na chuo cha ubaharia DMI na vyuo vingine ili kuweza kutumia fursa zilizopo katika fani hiyo kwani takwimu zinaonyesha kwa sasa taifa linamabaharia ambao wana umri mkubwa.
Kwa upande wake Kapteni Haruna Alli ambaye ni mkufunzi wa mafunzo kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam alisema mafunzo yamewajenga zaidi ili kuendana na kasi ya Dunia katika fani ya ubaharia itakayowezesha kuzalisha mabaharia wenye vigezo vya ushindani dunia.
Mafunzo hayo yalishirikisha washiriki selasini na tano kutoka taasisi za TASAC,Chuo cha DMI na wizara ya ujenzi na sekta ya uchukuzi yakifadhiliwa na shirika la Bahari Duniani (IMO)yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo walimu wa walimu ambao kazi yao kubwa ni kuwaelekeza watu wengine ili kuweza kupata wataalam wengi zaidi ambapo washiriki wote walipatiwa vyeti vya ushiriki.