Na Mwandishi waetu Siha.
SEKTA ya utalii imeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa, baada ya mashindano ya michezo ya pikipiki, baiskeli na riadha yanayojulikana kama West Kili Tour Challenge kufanyika kwa mafanikio katika misitu ya West Kilimanjaro, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro na kuvutia zaidi ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi.
Tukio hilo la siku mbili, lililofanyika kuanzia Juni 21 hadi 22, 2025, limeelezwa kuwa kichocheo cha ongezeko la watalii katika misitu ya hifadhi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na hivyo kusababisha mapato ya taasisi hiyo kupanda kutoka Sh154 milioni mwaka 2021 hadi Sh2 bilioni, ongezeko la mara 13.
Mkuu wa Dawati la Utalii nchini, Someni Mteleka, amesema tukio hilo limekuwa mfano bora wa jinsi utalii wa ndani unavyoweza kutumika kuongeza kipato cha taifa na kuhamasisha uhifadhi:
“Kwa sasa asilimia 80 ya watalii wanaotembelea misitu ya TFS ni Watanzania. Tukiendelea kuandaa matukio ya michezo kama haya, tutavuka watalii 500,000 na tutavuna mapato ya Sh5 bilioni kwa mwaka.”
Mashindano hayo yamehusisha mbio za pikipiki (km 75), baiskeli za milimani na riadha za kilomita 5, 10 na 21 zilizopita katika mandhari ya asili ya misitu ya West Kilimanjaro, yenye kuvutia kwa maporomoko ya maji, mashamba ya miti na mandhari ya milima.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Moshi,Godfrey Mnzava, amesema tukio hilo ni jukwaa la kimkakati la kuunganisha sekta ya michezo, biashara, utalii na burudani:
“Tumeshuhudia umati wa watu wakicheka, wakifanya biashara na wakifurahia mazingira ya asili. Msimu ujao tunapanga kuongeza michezo zaidi.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka, ametoa wito kwa Watanzania kutumia fursa ya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi za asili badala ya kuziona kuwa za wageni pekee.
Naye Mhifadhi Mkuu wa TFS Wilaya ya Siha, Robert Faida, amesema mafanikio ya mwaka huu ni uthibitisho kuwa utalii wa michezo unapaswa kupewa kipaumbele:
“Mwaka huu pekee tumepokea washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali. Tunaendelea kuboresha miundombinu na huduma kwa wageni ili kuvutia zaidi.”
Katika mashindano ya West Kili Tour Challenge, mshindi wa kwanza kwenye mbio za pikipiki zilizovutia hisia za mashabiki, Kelvin Gabriel, amezawadiwa Sh200,000. Nafasi ya pili ikienda kwa Liens Aron aliyepata Sh150,000, huku Msafiri akijishindia Sh100,000 kwa kumaliza wa tatu.
Katika mbio za riadha kilomita 21 kwa wanawake, Panuelia Katesigwa ameibuka kidedea akichukua nafasi ya kwanza, akifuatiwa na Consolata Lyimo aliyeshika nafasi ya pili, huku Grace Kapama akikamata nafasi ya tatu.
Kwa upande wa wanaume, Nicodem Joseph aling’ara kwa kushika nafasi ya kwanza, Jamal Said akaibuka wa pili na Tumaini Habie akakamilisha tatu bora
Katika mbio za baiskeli, Diego John ametwaa ushindi kwa kutumia saa 1:26, akifuatiwa kwa karibu na Abdul Bango aliyetumia saa 1:27, huku Nickson Lomayan akichukua nafasi ya tatu kwa kutumia saa 1:30.
Wadau wa utalii wamesema West Kili Tour Challenge msimu wa tano imeonesha uwezo mkubwa wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira, kukuza biashara ndogondogo na kulinda mazingira kupitia matumizi endelevu ya maliasili.
Mwisho